KAMANDA wa polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi amepiga marufuku kitendo cha askari wa usalama barabarani (Traffic) kuwatoza madereva Sh 9,000 kama malipo ya kusafisha njia ili wasikamatwe tena kwa makosa mbalimbali.
Kauli ya kamanda huyo, imekuja baada ya madereva wa daladala jijini Mbeya kutoa malalamiko katika mkutano baina yake na wamiliki na madereva wa jijini hapa, uliofanyika ukumbi Rayol Zambezi.
Madereva hao, walitoa kero zao katika risala yao kwamba wamekuwa wakitozwa Sh9,000 na trafiki kwa madai ya kusafisha njia na Sh1,000 kila kituo ambako wamesimama.
“Nimesikia kero zenu nyingi, lakini nasema hivi mbele yenu utaratibu wa kusafisha njia kwa Sh9,000 ukome kuanzia leo na kutoa Sh1,000 hiyo ni rushwa hivyo mambo haya yasijirudiwe tena,”alisema Kamanda Nyombi.
Nyombi alisema kitendo cha dereva au kondakta kutoa Sh1,000 ni kosa la jiani kwani mtoa rushwa na wanaopokea wote hao ni wahalifu na kwamba makondakta wamekuwa wakichochea kutoa rushwa ya Sh1,000 kwa trafiki ili kukwepa makosa ambayo wanafanya ikiwa ni pamoja na kujaza abiria na ubovu wa magari yao.
Kamanda aliwataka madereva hao, kufuata kanuni, taratibu na sheria za usalama barabarani ili kuondokana na migogoro baina yao na jeshi la polisi.
Katika hatua nyingine kwenye mkutano huo, Mchungaji William Mwamalanga alipewa bahasha ya fedha kwa kazi aliyoifanya ya kuwakutanisha madereva hao na jeshi la polisi.
“Unajua afande RPC mimi nilijua nafanya kazi hii kwa kujitolea, lakini nimeweza kupata hii bahasha nawashukuru hawa madereva kumbe unaweza ukafanya kazi na mshahara ukaupata baada ya kazi hiyo,”alisema Mchungaji huyo.
Mwananchi.co.tz
Brandy Nelson,
Mbeya
No comments:
Post a Comment