1 February 2011

WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli amefichua ufisadi wa TSh 5 billioni


Magufuli alipotembelea Mradi Wa Ujenzi Wa Babarabara Ya Jet Lumo
Picha kwa hisani ya http://mjengwa.blogspot.com/

WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli amefichua ufisadi wa Sh5 bilioni uliotaka kufanywa katika manispaa tatu za jijini Dar es Salaam kwenye ulipaji wa fidia za ubomoaji wa nyumba kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara.


Mbali na kufichua ufisadi huo jana, Magufuli ameagiza jengo la Wakala wa Barabara (Tanroads) lililopo ndani ya Kituo cha Daladala cha Ubungo, libomolewe ndani ya siku tano kuanzia jana kwa kuwa lipo ndani ya hifadhi ya kituo cha mabasi yaendayo kasi.


Dk Magufuli aligundua uozo huo na kutoa maagizo ya utekelezaji jana katika ziara yake ya kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa Dk Magufuli, majengo ya ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini humo, nayo yapo ndani ya hifadhi ya barabara jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Barabara Namba 167 ya mwaka 1967.
Akizungumza kabla ya kuanza ziara hiyo, Dk Magufuli alisema kuwa Serikali haikuridhika na tathimini ya kwanza iliyofanywa na wathamini kutoka Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke na kuthibitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali.


“Gharama za tathmini hiyo ilikuwa Sh27.7 bilioni kwa mali na nyumba 1,487. Lakini kabla ya kulipa, wizara iliona vyema kujiridhisha kwa kutembelea eneo la tathimini husika na kugundua mapungufu kadhaa,” alisema Magufuli na kuongeza:
“Mapungufu hayo ni pamoja na kurukwa kwa baadhi ya mali na nyumba pamoja na gharama za nyumba zenye sifa sawa kutofautiana kutoka manispaa moja na nyingine.”


Baada ya kugundua mapungufu hayo, Dk Magufuli alisema Wizara ilimtafuta mthamini wa kujitegemea ‘Independent Valuer’ ili afanye uhakiki na kurudia uthamini pale ilipohitajika kwa maslahi ya taifa.


"Unajua ilikuwaje? Nyumba zipatazo 61 zenye thamani ya Sh 239,781,542 hazikuonekana, kati ya hizo nyumba 56 zipo katika eneo la barabara ya Jet Corner-Vituka-Davis Corner na nyumba tano ziko eneo la kati ya stendi ya mabasi ya Ubungo na Kigogo,” alisema Magufuli.......endelea hapa

chanzo: Mwananchi.co.tz

No comments: