6 January 2011
KILICHO TOKEA NDANI YA CCM BAADA YA RUHSA YA MAANDIKO MAPYA YA KATIBA
Na Raymond Kaminyoge
BARAZA la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, limempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuandikwa upya kwa katiba ya Tanzania, huku wakilaani nguvu kubwa iliyotumika kumshinikiza akubaliane na suala hilo.
Wazee hao, wengi wakiwa ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walieleza msimamo wao huo jana jijini Dar es Salaam walipokutana na waandishi wa habari.
Tamko hilo lililojaa shutuma dhidi ya makundi ya watu yaliyomshinikiza Rais Kikwete hadi kufikia hatua hiyo, lilisomwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo ambaye pia ni mwanachama wa CCM, Mohamed Mtulia.
Kitendo cha baraza hilo kuwabeza kwa kuwalaani wale walioongoza mjadala wa kudai katiba mpya, kinatafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa ni wazee hao kwa upande mwingine kutofurahishwa na hatua Rais Kikwete kukubali suala hilo. Baadhi ya vyombo vya habari (siyo Mananchi) tayari vimeripoti kuwepo wahafidhina ndani ya CCM ambao hawakufurahishwa na hatua ya rais kuruhusu kuanza kwa mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.
Katika mkutano huo wa jana, Mtulia alianza kusoma tamko hilo kwa kumwagia sifa Rais Kikwete akisema kama baraza, wamefurahishwa na hatua aliyoichukua kuhusu mjadala wa katiba. “Baraza la wazee kwa niaba ya wazee wenzetu tumeamua kutamka hadharani kuwa tumefurahishwa na uamuzi wa Rais Kikwete kwa kukubali kuandikwa katiba mpya,”alisema Mtulia.
Mbali na kumpongeza Rais Kikwete kwa hatua hiyo, Mtulia akaonya kuwa katika kufikia suala hilo, isitumike jazba, kejeli, wala viherehere. “Tunawasihi watanzania wenzetu kusukumwa na utaifa, utu na ustaarabu katika kuitafuta na kuipata katiba mpya , jazba, kejeli viherehere na vitisho haviwezi kutupatia Katiba mpya,” alisema. Baadhi ya watu waliohudhuria mkutano huo ambao ni makada wa CCM ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi, Waziri wa zamani, Iddi Simba na Mwenyekiti zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Hemed Mkali.
Alisema kuwa katika harakati za kushinikiza katiba mpya dalili zinazoonyesha kuwepo kwa baadhi ya makundi ya watu wanaodhani kwamba wao wanaihitaji zaidi kuliko wengine. "Pia wapo wengine wanaodhani mawazo na matakwa yao pekee ndiyo yanayostahili kuingia kwenye katiba bila hata kujua katiba iliyopo.
"Zote ni dosari zinazoweza kupelekea kazi yetu ya katiba mpya isiwe na mafanikio. Sisi wazee tunaomba ieleweke kuwa katiba siyo pembejeo ya kilimo ambayo inamhusu mkulima pekee na kutomhusisha mvuvi bali katiba ni mwongozo wetu Watanzania wote. Mtulia aliwageukia viongozi wa dini na kusema: “Hakuna sababu ya kulifanya suala la Katiba mpya kuwa suala la kidini, kiasi cha kuligeuza kuwa ndiyo mahubiri au mawaidha ya msingi katika ibada kwa kuwa hata wenye imani tofauti au wasio na dini na wao inawahusu,” alisema.
Hakuwaacha kando wanasiasa ambao walikuwa mstari wa mbele katika vuguvugu hilo akiwakemea kwa kusema: "Hakuna sababu ya kusukumwa na jazba wala kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa kuwa hata wasio wanasiasa wanaguswa na katiba mpya." Kama lengo ni kupata katiba mpya, Mtulya ambaye wakati wote alikuwa akishangiliwa na wazee waliofika kuunga mkono azimio hilo, alisisitiza: "Njia bora ya kufikia lengo (la katiba mpya) ni kuwa pamoja, kuweka mbele utu, maslahi ya taifa na haki ya kila mmoja wetu.
Kauli hiyo ya wazee imekuja wakati ambao viongozi wa dini na vyama vya siasa vikipongezana kwa mafanikio waliyoyapata baada ya kuongoza mjadala wa kudai katiba mpya hadi Rais Kikwete kutangaza kwamba mwaka 2011 mchakato wake utaanza. Desemba 31 mwaka jana Rais Kikwete alitangaza kukubali kuandikwa kwa katiba mpya na kuahidi kuunda tume itakayoongozwa na mwanasheria aliyebobea ili kuongoza mchakato wa katiba mpya.
Hatua hiyo aliichukua baada ya vyama vya siasa vya upinzani, CUF, Chadema, TLP kutamka hadharani malengo yao ya kutaka katiba mpya. Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alikuwa tayari ametangaza nia yake ya kupeleka Bungeni hoja binafsi ya kutaka katiba mpya.
Hata hivyo, hivi karibuni aliliambia gazeti hili kwamba amesitisha nia hiyo ili kuona matokea ya mchakato uliotangazwa na Rais Kikwete. Katika kushinikiza katiba mpya, wanachama wa CUF waliandamana kwenda kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Komban licha ya polisi kukataa kuyaidhinisha na kusema ni batili. Wasomi na wanasheria nchi nao walijiingiza katika vuguvugu hilo na kuishauri serikali kukubali mkakati huo wa katiba mpya kwa sababu iliyopo imepitwa na wakati na haikidhi matakwa ya sasa.
Chanzo:mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment